Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changisho la dola milioni 497 lazinduliwa kwa usaidizi wa dharura Iraq

Changisho la dola milioni 497 lazinduliwa kwa usaidizi wa dharura Iraq

Wakati mapigano yakishika kasi nchini Iraq, Umoja wa Mataifa umezindua ombi la changisho la takriban dola milioni 500, ili kuwezesha upatikanaji wa makazi, chakula, maji safi na huduma nyingine muhimu kwa kipindi cha miezi sita ijayo.Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Wakati wa kuzindua ombi hilo la changisho mjini Brussels, Ubelgiji, Msaidizi wa Katibu Mkuu na Naibu Mratibu wa Masauala ya Kibinadamu, Kyung-Wha Kang, amesema zaidi ya raia milioni 8 wa Iraq sasa wanahitaji misaada na ulinzi wa dharura.

Amesema ingawa Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wamekuwa wakitoa misaada, programu za utoaji misaada sasa inakabiliwa na upungufu wa ufadhili, na hivyo kutishia kukatiza asilimia 50 ya jitihada za utoaji misaada.

Msemaji wa changisho hilo ni Simon Ingram, ambaye ni Msemaji Mkuu wa shirika la UNICEF, ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini

“Changisho hili linalenga tu kufadhili mahitaji ya dharura, ya kuokoa maisha ya watu wapatao milioni tano na nusu kwa miezi sita ijayo. Kuna upungufu mkubwa sasa, kwa hiyo zinahitajika kwa sababu baadhi ya huduma muhimu, kama za afya na chakula, zinakwama na hata kufungwa kwa sababu fedha zinakwisha.”

Tayari kliniki 77 muhimu zimefungwa na mgawo wa chakula kupunguzwa kwa zaidi ya watu milioni moja.