Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali ya Yemen

Baraza la Usalama lajadili hali ya Yemen

Wakati sintofahamu nchini Yemen ikiendelea, wananchi wake wakiendelea kusaka hifadhi nchi jirani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linakuwa na kikao cha faragha kuhusu hali ilivyo nchini humo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kikao hicho cha faragha kinapatiwa muhtasari wa hali halisi kutoka kwa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, atakayehutubia kwa njia ya video kutoka Sana’a.

Mashauriano hayo ya faragha yanafanyika takribani saa 12 baada ya Baraza la usalama kutoa taarifa yake inayosihi wadau wote wa Yemen kushiriki kwenye mazungumzo ya kurejesha amani haraka iwezekanayo.

Wajumbe wa baraza katika taarifa hiyo walieleza masikitiko yao kuwa mashauriano yaliyopangwa kufanyika tarehe 28 mwezi uliopita huko Geneva, hayakufanyika licha ya hali mbaya ya kisiasa na kibinadamu nchini Yemen.

Wamerejelea maazimio ya baraza hilo yakitaka kufanyika kwa mchakato wa amani na jumuishi ili Yemen irejee katika hali ya amani wakisema kuwa wanaunga mkono jitihada za Bwana Ahmed na kwamba mchakato wa suluhu ya mzozo Yemen iongozwe na wayemeni wenyewe wakitambua umoja, na utaifa wa nchi hiyo.