Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaendelea na kampeni ya kila mtoto Sudan Kusini aende shule

UNICEF yaendelea na kampeni ya kila mtoto Sudan Kusini aende shule

Kampeni ya kitaifa ya kuhakikisha watoto wote Sudan Kusini wanakwenda shule imezinduliwa jimbo la Equitoria Magharibi nchini humo ikiwa ni eneo la mwisho kufanya hivyo baada ya maeneo mengine kukamilisha uzinduzi huo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema lengo ni kubadili mwelekeo wa watoto kuacha kwenda shule na badala yake waende na wasome kwa kuwa elimu ni haki ya msingi ya mtoto bila kujali anaishi mazingira ya mzozo au la.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo mjini Yambio, Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini Jonathan Veitch amesema mzozo unaoendelea unazidi kuzorotesha uchumi lakini elimu ni suala la uokozi wa maisha kwa kuwa mtoto ambaye mama yake anajua kusoma ana uwezo wa kuishi zaidi ya umri wa miaka mitano.

Hata hivyo mpango huo wa elimu Sudan Kusini unakumbwa na mkwamo ambapo umechangia asilimia 21 tu kwa mwaka huu, lakini serikali ya Japan imechangia dola Milioni 9.5 kusaidia miradi ya UNICEF nchini humo ikiwemo ile ya elimu.

Kampeni hiyo ya kitaifa ya elimu imeanza mwezi Februari ikilenga watoto 400.000, gharama yake ni dola Milioni 42 na lengo la ni kuhakikisha watoto watoro shuleni wanarejea na wale ambao hawakuwahi kwenda shule wanafanya hivyo hasa kwenye maeneo yenye mizozo.