Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi: Mkuu wa maswala ya kisiasa wa UM aomba kurejeshwa kwa mazungumzo

Burundi: Mkuu wa maswala ya kisiasa wa UM aomba kurejeshwa kwa mazungumzo

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maswala ya kisiasa, Jeffrey Feltman, amekutana Jumatatu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombanza, aliyekuwa ziarani Marekani kwa ajili ya mkutano kuhusu mabadiliko ya idadi ya watu duniani. Hayo ni kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, akizungumza na waandishi wa habari mjini New York.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Bwana Feltman amemwambia Makamu huyo wa Rais kwamba mapendekezo yaliyotolewa na Kikao cha viongozi wa Afrika Mashariki yameipa serikali ya Burundi fursa mpya ya kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi wenye amani na utakaoaminika.

Bwana Feltman amependekeza serikali ya Burundi ichukue fursa hii na kuchukua hatua za kuonekana, hasa kuhakikisha usalama wa mchakato wa uchaguzi, usalama wa wadau wa kisiasa na kijamii, pamoja na kusalimisha raia waliojihami, na kuimarisha Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi, na hatimaye, kuwezesha wakimbizi kupiga kura.

Aidha Bwana Dujarric amesema kuwa Feltman ameiomba serikali ya Burundi ianze tena kushiriki kwenye mazungumzo ya kisiasa na kwa nia nzuri, akiongeza:

(Sauti ya Dujarric)

“ Tunaendelea kuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa ghasia na tunakariri wito wetu wa amani na utulivu. Tunawasihi Warundi kueleza maoni yao kwa njia ya amani na tunaviomba vyombo vya usalama kujiepusha na kutenda ukatili wakati wa kudhibiti maandamano. Tunazingatia pia haki ya Warundi ya kueleza maoni yao, tukiwasihi kufanya hivyo kwa njia ya amani.”

Aidha Bwana Dujarric amesema kwamba Katibu Mkuu Ban Ki-moon amezungumza na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete Jumatatu kwa njia ya simu, akimpongeza kwa uongozi wake katika jitihada za kutatua mzozo huo.