Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Milioni 15 za CERF kusaidia wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda na Tanzania

Dola Milioni 15 za CERF kusaidia wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda na Tanzania

Mratibu Mkuu mpya wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien ametangaza kutoa dola Milioni 15 kutoka mfuko wa dharura wa umoja huo, CERF kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchi jirani za Rwanda na Tanzania.

Bwana O’Brien amesema takribani dola Milioni 7.5 zitaelekezwa Tanzania kwa kuimarisha msafara wa wakimbizi wapya kutoka mpakani kupitia vituo vya mpito vya mapokezi hadi kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.

Kiasi kilichobakia cha takribani dola Milioni Nane kitaelekezwa Rwanda ambako kisaidia operesheni za kuimarisha uokozi wa binadamu ikiwemo mahitaji katika vituo viwili vya mapokezi na kambi ya Mahama..

Hata hivyo Bwana O’Brien ambaye pia ni mkuu wa Ofisi ya OCHA amesema anatarajia kupata misaada zaidi kwani mashirika ya misaada nchini Tanzania yameonya kuwa hali ya maisha kwa wakimbizi ni mbaya na inatia hofu ya kuhatarisha afya.

Tangu mwezi Aprili, zaidi ya watu 70,000 wengi wao wakiwa watoto wamelazimika kukimbia Burundi kutokana na mzozo wa kisiasa na kukimbilia nchi jirani ambapo 46,000 wako Tanzania na 26,000 wako nchini Rwanda.