Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marufuku kuvuta sigara katika majengo yetu: UNRWA

Marufuku kuvuta sigara katika majengo yetu: UNRWA

Kuanzia hii leo bango lenye ujumbe wa makataaa ya matumizi ya tumbaku litakuwa linaonekana katika maeneo yanayomilikiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA imesema taarifa ya shirika hilo.

UNRWA inasema tangazo hilo linakwenda sambamba na mapendekezo ya shirika la afya ulimwenguni WHO ambapo msisitizo wa marufuku ya matumizi ya tumbaku katika maeneo ya UNRWA inasisitiza kuwa ndani au nje ya majengo ya shirika hilo matumizi hayo yamezuiwa isipokuwa kwa maeneo maalum yanayoruhusiwa.

Shirika hilo limesema tangu mwaka 2006 limekuwa katika harakati za kupiga marufuku matumizi ya uvutaji wa sigara pale ambapo uvutaji huo ulipopigwa marufuku ndani ya majengo na magari ya UNRWA na kuruhusiwa nje, ambapo sasa sera hiyo inarekebishwa ili kupiga marufuku nje ya majengo pia.

Taarifa hiyo imesema kuwa maamuzi hayo yatawezesha mazingira yasiyo na uvutaji wa sigara kwa wakimbizi wa Kipalestina ambao wanatumia huduma za UNRWA kama vile shule, vituo vya afya, vituo vya kijamii na majengo mengine na kuongeza kuwa mfanyakazi atakayekiuka masharti hayo ataadhibiwa.