Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani uamuzi wa Sudan Kusini kumfukuza Toby Lanzer

Ban alaani uamuzi wa Sudan Kusini kumfukuza Toby Lanzer

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani uamuzi wa serikali ya Sudan Kusini kumfukuza Naibu Mwakilishi wake maalum nchini humo, Toby Lanzer. Bwana Lanzer amekuwa pia Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Ban akimsifu Bwana Lanzer kwa juhdi zake katika kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya kibinadamu ya jamii zilizoathiriwa na mgogoro nchini humo, na kwa kuhakikisha kuwa usaidizi wa kunusuru maisha unawafikia wale waliomo hatarini zaidi. Ban amesema juhudi hizo zimekuwa muhimu kwa sababu ya kuendelea machafuko, pande kinzani zikiwa zimeshindwa kufikia makubaliano ya kina ya amani.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini kubadili uamuzi huo mara moja, na kuisihi ishirikiane kikamilifu na wawakilishi wote wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Tayari Katibu Mkuu amemteua mrithi wa nafasi ya Bwana Lanzer, ambaye alikuwa anakaribia kumaliza muda wake.