Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sintofahamu Burundi, Ban kuzungumza na Rais Kikwete wa Tanzania

Sintofahamu Burundi, Ban kuzungumza na Rais Kikwete wa Tanzania

Umoja wa Mataifa umesema umekuwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa chaguzi huru, haki na shirikishi kufanyika nchini Burundi katika mazingira ya sasa wakati huu ambapo serikali nchini humo imetangaza kuwa uchaguzi wa wabunge utafanyika baadaye wiki hii kama ilivyopangwa.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema hayo wakati akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kufahamu msimamo wa Umoja huko kuhusu hatua ya Burundi juu ya uchaguzi wa wabunge na Rais.

Amesema Mjumbe maalum wa Umoja huo kwa maziwa makuu Said Djinnit anaendelea na harakati za kukutana na pande zote  husika kwenye sintofahamu inayoendelea Burundi, sambamba na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye..

(Sauti ya Farhan)

Naamini anatarajia kuwasiliana baadaye leo na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ili kupata habari kamili kuhusu hali ilivyo sasa. Lakini hatimaye hili ni jambo ambalo linapaswa kuridhiwa na pande zote. Hata hivyo tunahitaji kuhakikisha vyovyote watakavyokubaliana, wataafikiana kuwa chaguzi zinazofanyika zinakuwa salama, halali na jumuishi.”

Alipoulizwa msimamo wa Umoja wa Mataifa kufuatia kauli ya msemaji wa serikali ya Burundi kuwa suala la awamu ya tatu ni la mamlaka ya nchi na si vinginevyo na hivyo hoja imefungwa, Bwana Haq amesema Umoja wa Mataifa umekuwa unaeleza bayana kuwa makubaliano ya Arusha ni lazima yazingatiwe na kwamba wananchi wa Burundi wenyewe wanaweza kukubaliana kuhusu mustakhbali wao juu ya chaguzi huru, salama na haki.