Mistura aendelea na mashauriano kuhusu Syria huko Geneva.

1 Juni 2015

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa suala la Syria, Staffan de Mistura ameendelea na mashauriano kuhusu mzozo wa nchi hiyo huko Geneva, Uswisi.

Taarifa zinasema kuwa leo Jumatatu amekuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Ufalme wa Bahrain ukiongozwa na mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa Yusuf Abdulkarim Bucheeri.

Bwana Bucheeri ameelezea mtazamo wake kuhusu suluhu la kisiasa la mzozo wa Syria na kinachoendelea hivi sasa nchini humo.

Bwana Mistura ambaye pia amekuwa na mikutano ya ndani na watendaji wake kutoka Geneva, na Damascus, Syria amesema miaka minne ya ukatili utokanao na mzozo wa Syria ambao tayari umeingia mwaka wa tano hauwezi kumalizika kijeshi.

Kwa mantiki hiyo amesema ametumia vikao vya leo kusikia vile pande husika zinaguswa na umuhimu wa kumalizika kwa vita hivyo ambavyo vinaendelea kutiririsha damu ya wananchi wa Syria huku athari zake zikivuka mipaka siyo tu kikanda bali kimataifa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter