Skip to main content

Mitandao ya kigaidi ni ya kimataifa, ikabiliwe kimataifa- Amano

Mitandao ya kigaidi ni ya kimataifa, ikabiliwe kimataifa- Amano

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, Yukiya Amano, amesema kuwa mitandao ya kigaidi hutekeleza vitendo vyao katika mitandao ya kimataifa na hivyo basi inapaswa kukabiliwa kwenye ngazi ya kimataifa.

Bwana Amano amesema hayo wakati kongamano la kimataifa kuhusu teknolojia ya kompyuta katika ulimwengu wenye nishati ya nyuklia, ambalo limeanza leo katika makao makuu ya IAEA mjini Vienna, Austria.

Amesema ingawa usalama wa nyuklia ni wajibu wa kitaifa, IAEA ikiwa na nchi wanachama 164, ina wajibu muhimu katika kuusaidia ulimwengu kuchukua hatua za pamoja dhidi ya tishio la ugaidi wa kutumia nishati ya nyuklia.

(Sauti ya Yukiwa Amano)

“Magaidi na wahalifu wengine hutekeleza vitendo vyao katika mitandao ya kimataifa, na wanaweza kushambulia popote. Kwa hiyo kupambana nao ni lazima kuwe kwa kimataifa.”

Hii ni mara ya kwanza kongamano kuhusu suala la usalama wa kompyuta katika nyuklia linafanyika kwenye IAEA, likiwaleta pamoja zaidi ya wataalam 650 kutoka nchi zinazozidi 100.