Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi zaidi wahitajika kuhusu uhalifu uliofanywa na askari wa kimataifa CAR: ZEID

Uchunguzi zaidi wahitajika kuhusu uhalifu uliofanywa na askari wa kimataifa CAR: ZEID

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad al Hussein amezisihi nchi mbali mbali kuongeza jitihada ili kuchunguza kuhusu madai ya vitendo vya ukiukaji wa haki na mauaji ya raia vinavyodaiwa kufanywa na askari wa kimataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu, Kamishna Zeid amenukuliwa akisema madai hayo yanasikitisha sana, akiongeza kwamba hata kama baadhi ya nchi zimeshafukuza askari walioshukiwa kujihusisha na mauaji hayo, bado hatua zingine zinahitajika ili kuhakikisha vitendo kama hivyo havitokei tena.

Baadhi ya askari wa Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini CAR, MISCA, wanadaiwa kujihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu, mauaji ya raia, na utumikishwaji wa kingono wa wanawake na watoto, mwaka 2014.

Ripoti ya awali kuhusu uhalifu huo iliwasilishwa na watalaam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Disemba mwaka 2014, na ripoti nyingine kuhusu vitendo hivyo inatakiwa kutangazwa wiki ijayo.