Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji bora wahitajika kunufaika na mabadiliko ya mfumo wa idadi ya watu duniani:

Uwekezaji bora wahitajika kunufaika na mabadiliko ya mfumo wa idadi ya watu duniani:

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya juu kubaini fursa za uwekezaji zinazotakiwa ili kunufaika na mabadiliko ya mwelekeo wa mfumo wa idadi ya watu duniani wakati huu ambapo idadi ya vijana inaongezeka halikadhalika wazee. Taarifa Zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Sam Kutesa ambaye ni Rais wa Baraza hilo katika hotuba yake amenukuu takwimu ambazo zinaonyesha kuwa kati ya vijana bilioni Moja nukta Nane duniani kote, Tisa kati ya Kumi wako Afrika ambapo nchi zao zikiweka mikakati na sera sahihi zinaweza kuwajumuisha kwenye ajira zitakazobadilisha maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ban Ki-,moon amesema katika dunia ya leo ambayo vijana Milioni 74 hawana ajira ni tatizo kubwa kwa hiyo akatoa mapendekezo manne.

(Sauti ya Ban)

“Mosi tuhakikishe huduma za uzazi wa mpango zinapatikana ili kuepusha magonjwa ya kuambukiza na mimba zisizohitajika, pili vijana wapate elimu bora na mafunzo na tatu tunahitaji mafunzo yanayoratibiwa yakizingatia haki za binadamu na utu, na nne hifadhi ya jamii ya kuondoa umaskini na ukosefu wa usawa.”

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi waandamizi akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi na mawaziri kutoka nchi wanachama wa Umoja huo.