Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wakaribisha kuondolewa kwa adhabu ya kifo Nebraska, Marekani

Umoja wa Mataifa wakaribisha kuondolewa kwa adhabu ya kifo Nebraska, Marekani

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, imekaribisha kupigwa marufuku kwa adhabu ya kifo katika jimbo la Nebraska, mnamo Jumatano wiki hii, na hivyo kulifanya jimbo hilo kuwa la 19 kote nchini Marekani kufanya hivyo.

Jimbo la Nebraska halijatekeleza adhabu ya kifo dhidi ya mfungwa yeyote tangu mwaka 1997. Kwa ujumla, idadi ya watu wananyongwa Marekani kila mwaka na idadi ya watu wanaopewa hukumu ya kifo imekuwa ikipungua taratibu kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Mnamo mwaka 2014, adhabu ya kifo Marekani ilitekelezwa katika majimbo 7 pekee, huku idadi ya watu waliouawa ikiwa 35, ambayo ndiyo ya chini zaidi tangu mwaka 1994.

Ofisi ya Haki za Binadamu imesema, inatumai kuwa mfano wa Nebraska utaigwa na majimbo mengine ya Marekani (yakiwemo Colorado, Delaware, Montana na Kansas) ambako mabunge yanajadili kuhusu kupigwa marufuku adhabu ya kifo, na kukariri pendekezo la Kamati ya Haki za Binadamu kwa serikali ya Marekani kuwa isitishe adhabu kifo kwa ngazi ya kitaifa.