Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amos alitaka Baraza la Usalama liwajali raia wa Syria

Amos alitaka Baraza la Usalama liwajali raia wa Syria

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Valerie Amos, amewataka wajumbe wa Baraza la Usalama waweke kando tofauti zao kisiasa na kutafutia suluhu mzozo wa Syria na kwa ajili ya vizazi vya nchi hiyo vijavyo.

Bi Amos ambaye amekuwa akilihutubia Baraza hilo kwa mara ya mwisho kama Mkuu wa OCHA, amesema katika kipindi cha zaidi ya miaka minne, taifa la Syria limetumbukia katika hali ya kutokuwa na matumaini, na kwamba hali nchini humo inazorota kila uchao.

Katika wiki zilizopita, tumeona vitendo vya uovu zaidi. Wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia wakuawa, kulemazwa, kulazimika kuhama makwao na kutendewa unyama ambao mwanadamu yeyote hastahili kutendewa.”

Bi Amos amesema, kufikia sasa, zaidi ya watu milioni 12.2 wanahitaji usaidizi wa dharura nchini Syria, na wale ambao walikuwa wanaweza kujitegemea, sasa hawawezi kumudu kujikimu tena kimaisha.

Watoto milioni mbili hawaendi shule nchini Syria. Gharama za janga hili kijamii, kiuchumi na kibinadamu ni kubwa. Huenda ikachukua vizazi kadhaa kwa Syria kujikwamua tena…. Hatuwezi kuwatelekeza Wasyria hadi wakate tamaa”

Ametoa wito kwa Baraza la Usalam kuchukua hatua ili kuwalinda raia, na kuhakikisha kuwa pande zinazozozana zinatimiza wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa, kuwawajibisha wanaokiuka sheria hiyo, na kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia wote wenye mahitaji nchini Syria.