Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNMISS

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNMISS

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wameptisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wake nchini Sudan Kusini, UNMISS, hadi Novemba 30, 2015.

Baraza hilo limetoa mamlaka kwa UNMISS kutumia njia zote kulinda raia kutokana na hatari ya ukatili, bila kujali ukatili huo unatekelezwa na nani, na kuzuia utendaji wa ukatili dhidi ya raia, wakiwemo raia wa kigeni. UNMISS pia imepewa mamlaka kutekeleza mkakati wa kutoa onyo mapema katika ujumbe wake mzima, na kuimarisha usalama wa umma kwenye maeneo yake ya ulinzi wa raia.

Kwa kuzingatia kuwa hali nchini Sudan Kusini inaendelea kutishia amani ya kimataifa na usalama wa kikanda, Baraza hilo limekariri uungaji wake mkono makubaliano yaliyosainiwa na serikali ya Sudan Kusini na waasi wa SPLM/A Upinzani mnamo Januari 23, pamoja na makubaliano ya kutatua mzozo nchini humo yaliyosainiwa mnamo Mei 9 2014.

Baraza la Usalama pia limetoa wito makubaliano hayo yatekelezwe mara moja kikamilifu na pande zote katika mzozo wa Sudan Kusini.