Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi ihakikishe inakomesha machafuko: Feltman

Burundi ihakikishe inakomesha machafuko: Feltman

Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amekutana na mwambata wa Waziri Mkuu wa Burundi katika juhudi za kusaka suluhu ya sintofahamu iliyoikumba nchi hiyo takriban mwezi mmoja uliopita, ambapo amesisitiza umuhimu wa serikali kuzuia  kuendelea kwa machafuko ya kisiasa na mauaji pamoja na machafuko yanayowalenga waandishi wa habari na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Akiongea na waandishi wa habari mini New York msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Stephane Dujarric  amesema kuwa Feltman ametaka kuwepo kwa usalama katika mchakato wa uchaguzi, wadau wa siasa pamoja na asasi za kiaraia huku pia akisisitiza upokonywaji silaha miongoni mwa raia.

Amesema kuwa mkuu huyo wa  masuala ya ulinzi katika Umoja wa Mataifa amesisitiza  umuhimu wa kuimarishwa kwa tume huru ya kitaifa ya uchaguzi pamoja na kuheshimiwa kwa makubaliano ya Arusha. Dujarric amesema Bwana Feltman anahofia kuongezaka kwa machafuko na kusisitiza

(SAUTI DUJARRIC)

"Bwana Feltman amesisitiza kuwa hatari ya kuongezeka kwa machafuko inasalia na hivyo mshauri maalum wa kuepusha mauji ya kimbari Adama Dieng  amewasili mjini Bujumbura leo."

Katika hatua nyingine msemaji wa Katibu Mkuiu wa Uomja wa Mataifa amesema kuwa  hapo jana Bwana Ban amezungumza kwa simu na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete  na kulezea matumaini yake majadiliano ya kusaka amani nchini Burundi yatahuishwa hima na kuongeza kuwa ilikuwa muhimu kuwa wadau nchini humo kuchukua hatua muhimu katika kupunguza machafuko na mivutano ili kuruhusu uchaguzi wa haki.