Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwishoni mwa ziara, Ban asifu Ubelgiji na kumulika tabianchi na vijana

Mwishoni mwa ziara, Ban asifu Ubelgiji na kumulika tabianchi na vijana

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye amehitimisha ziara yake Ubelgiji, amelisifu taifa hilo kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kimataifa, ikiwemo mchango wake katika kuendeleza amani Jamhuri ya Afrika ya Kati, kupitia Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kujenga Amani.

Ban amesema Ubelgiji ni miongoni mwa nchi 20 zinazoongoza katika kuchangia bajeti ya Umoja wa Mataifa na ile ya ulinzi wa amani, na kuongeza kuwa msaada wa kimaendeleo wa Ubelgiji unasaidia kukuza maendeleo Afrika, haki za wanawake na ulinzi wa mazingira katika baadhi ya nchi zilizo hatrarini zaidi.

Aidha, Ban amemulika matukio matatu muhimu yanayotazamiwa kufanyika, ambayo ni muhimu kwa maendeleo endelebvu, yakiwa ni makongamano ya Addis Ababa, New York na Paris, akisema kuwa matukio hayo yanatoa fursa ya mwisho kwa wanadamu kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi na kutokomeza umaskini.

Ban ametoa pia ujumbe kwa vijana, akiwahimiza wawe raia wa dunia, wafanye kazi kwa shauku na fadhila, watoe changamoto kwa viongozi wao, kwa kuwaambia kuwa wana wajibu wa kuufanya ulimwengu kuwa wenye amani na ufanisi zaidi.