Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Yemen, Ban azungumza na Rais Hadi

Mzozo Yemen, Ban azungumza na Rais Hadi

Huku mzozo nchini Yemen ukizidi kushika kasi kila uchao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Abdrabuh Mansour ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mashambulio ya anga nan chi tangu tangu kumalizika kwa sitisho la muda la mapigano lililolenga kuwezesha huduma za kibinadamu.

Amerejelea wito wake kuwa hakuna suluhu la mzozo huo kwa njia ya mapigano akimsisitiza mjumbe wake maalum nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed kuongeza maradufu jitihada za mashauriano yake na pande zote ikiwemo serikali, vikundi vya kisiasa kwa lengo la kurejesha mashauriano ya Geneva haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo Ban ameshukuru azma ya Rais Hadi ya kuzingatia mazungumzo ya amani yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa na ushiriki wao kikamilifu kwenye mashauriano hayo ambayo Katibu Mkuu amesema anatumai yatarejea punde.

Mashauriano hayo yakihusisha pande zote kwenye mzozo wa Yemen yalikuwa yaanze tarehe 28 mwezi huu huko Geneva, lakini ilipofika tarehe 26 Mei Katibu Mkuu alimwomba mjumbe wake ayaahirishe kutokana na ombi la serikali ya Yemen na wadau wengine.