Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira umeongezeka kwa 25% miongoni mwa Wapalestina- ILO

Ukosefu wa ajira umeongezeka kwa 25% miongoni mwa Wapalestina- ILO

Ukosefu wa ajira miongoni mwa Wapalestina umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 25, kwa mujibu wa Shirika la Ajira Duniani, ILO.

ILO imesema kuwa ongezeko hili limesababishwa na mkwamo wa mchakato wa amani na Israel na athari za vita vya Gaza mwaka jana, 2014.

ILO imeongeza kuwa wafanyakazi Gaza na Ukingo wa Magharibi wanakumbwa na hali isotia matumaini kiajira na vitega uchumi.

Takwimu za ILO zinaonyesha kuwa, kati ya watu zaidi ya milioni nne, Wapalestina 338,000 sasa hawana ajira, huku viwango vya ukosefu wa ajira katika maeneo yaliyokaliwa vikiwa asilimia 27.

Zaidi ya Wapalestina 52,000 hufanya kazi kihalali Israel ambako kuna malipo ya juu, na wengine 26,000 hufanya kazi katika maeneo yaliyokaliwa.

Tariq Haq ni afisa wa ILO:

“Mishahara inayopatikana Israel ni zaidi ya mara mbili ya ile inayopatikana katika sekta binafsi Palestina, na hiyo inaonyesha ni kwa nini wafanyakazi wa Palestina watafanya lolote ili wafanye kazi katika uchumi wa Israel, hata ikimaanisha kuvumilia safari ngumu na mazingira hatarishi kwenye vituo vya upekuzi na maafa mengine wanayokumbana nayo.”

Hata hivyo, mazingira ya kazi katika sekta isiyodhibitiwa hayaridhishi, kwani aghalabu wafanyakazi wananyanyaswa, hususan katika bonde la Jordan.