Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Kiuchumi na Kijamii lakutana kuhusu kuimarisha mifumo ya afya

Baraza la Kiuchumi na Kijamii lakutana kuhusu kuimarisha mifumo ya afya

Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC, limekuwa leo na mkutano kuhusu ubia katika uimarishaji wa mifumo ya afya kwenye ajenda ya baada ya mwaka 2015. Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Mkutano huo unamulika jinsi ubia unavyoweza kuimarisha mifumo ya afya, na kujenga uthabiti dhidi ya majanga ya magonjwa ya kuambukiza.

Kikao kimemulika pia suala la ubia na mchango wake katika kutimiza ajenda ya maendeleo baada mwaka 2015.

Akihutubia kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesisitiza umuhimu wa ubia na njia mpya za kukabiliana na matatizo yaliyopo duniani sasa

Sauti ya Eliasson

Kutoka kwa mlipuko wa Ebola, hadi kuenea kwa misimamo mikali katili na ugaidi hadi hatari ya mabadiliko ya tabianchi hadi msururu usiokwisha wa migogoro, ni dhahiri kuwa hakuna taifa moja au shirika linaloweza kuyatatua matatizo haya peke yake. Naamini kuwa njia mpya ya kutatua matatizo unahitajika katika dunia ya leo. Ni lazima tuwe na ubia kwa ngazi zote: kitaifa, kikanda na kimataifa.”

Wengine waliohutubia ni Rais wa Baraza la ECOSOC, Martin Sajdik, na rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton.