Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi: Djinnit kuhutubia kwa njia ya video kutoka Bujumbura

Burundi: Djinnit kuhutubia kwa njia ya video kutoka Bujumbura

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa maziwa makuu, Said Djinnit mchana huu anahutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kutoka mji mkuu wa Burundi, Bujumbura katika kikao ambacho ni cha faragha.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameeleza kuwa kikao hicho kinafanyika wakati huu ambapo mashauriano ya kisiasa Burundi yaliahirishwa tarehe 24 mwezi huu kufuatia ombi la pande zote husika baada ya mauaji ya kiongozi wa upianzani nchini humo Zedi Feruzi.

Hata hivyo amesema ..

“Tunasisitiza wito wa utulivu na kujizuia na mamlaka za Burundi zizingatie haki za binadamu wa warundi wote na kushiriki katika hatua thabiti za kuzuzia mauaji kwa misingi ya kisiasa na ghasia zaidi. Bwana Djinnit ataendelea kushauriana na wadau wote Burundi ili kuhamasisha warejelee kwenye mazungumzo na kukubaliana hatua bora za kufanyika kwa uchaguzi huru, halali na jumuishi nchini Burundi.”

Bwana Dujarric amesema Umoja wa Mataifa unatumai kuwa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 31 mwezi huu utakuwa ni fursa ya kuchagiza mazungumzo baina ya warundi.