Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

De Mistura akutana na wajumbe wa Iran na UAE kuhusu Syria

De Mistura akutana na wajumbe wa Iran na UAE kuhusu Syria

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, amekutana leo na wawakilishi wa Iran na Milki za Kiarabu, UAE, akisisitiza umuhimu wa mchango wa nchi jirani za Syria katika kutafutia suluhu la kisiasa mzozo wa Syria, pamoja na haja ya kumaliza umwagaji damu mara moja.

Ujumbe wa Jamhuri ya Iran uliongozwa na Bwana Mohsen Naziri Asl, Mwakilishi wa Iran wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva. Balozi Asl amemwelezea Bwana de Mistura maoni ya serikali yake kuhusu mzozo wa Syria. Wamejadili pia kuhusu hali ndani ya Syria na katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Katika mkutano wake na wajumbe wa UAE, wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kuhusu Usalama na Masuala ya Kijeshi, Fares Al Mazrouei, wajumbe hao wameelezea maoni ya serikali UAE kuhusu mzozo wa Syria na kuhusu jinsi ya kuumaliza kupitia suluhu la kina la kisiasa.