Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manjoo ataka mazungumzo ili kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake Sudan

Manjoo ataka mazungumzo ili kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake Sudan

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, Rashida Manjoo, ametoa wito kuwepo mazungumzo ya wazi miongoni mwa pande zote katika mzozo nchini Sudan ili kukabiliana na vyanzo na athari za ukatili dhidi ya wanawake nchini humo. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

Taarifa ya Grace

Manjoo amesema mazungumzo hayo ya wazi yanapaswa kukabiliana na changamoto kama vile unyanyapaa wa kijamii na ukimya unaoambatana na aina fulani za ukatili, mazingira yasiyojali au wakati mwingine yasiyokuwa rafiki pale suala la ukatili dhidi ya wanawake linapotajwa, pamoja na kutoripoti, au kuripoti kwa kiwango cha chini visa vya ukatili na takwimu haba.

Mtaalam huyo ametaja pia desturi za kijadi, kitamaduni na kijamii ambazo huzuia kuripoti na kutafuta usaidizi kutoka kwa watu wasio jamaa wa wahanga wa ukatili, zikijikita kwa maridhiano badala ya uwajibikaji pale uhalifu unapotendwa dhidi ya wanawake na wasichana.

Ametoa wito kwa serikali ya Sudan na wadau wote kutafuta njia ya kufanya mazungumzo yatakayoondoa utata uliopo, hususan na jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa, kwa maslahi ya watu wa Sudan.