Baraza la usalama laangazia usalama wa waandishi wa habari kwenye mizozo

27 Mei 2015

Baraza la Usalama leo limekuwa na mjadala maalum kuhusu usalama wa waandishi wa habari vitani, huko wakizidi kukumbwa na hatari za ugaidi na mizozo ya siku hizi, waandishi 66 wakiwa wameuawa mwaka 2014 tu, nchini Sudan, Irak, Yemen, Ukraine na Syria.

Baraza hilo limepitisha azimio kwa kauli moja likilaani mauaji ya waandishi wa habari na kuzisihi nchi wanachama kuwajibika katika kutunza usalama wao na kupambana na ukwepaji wa sheria.

Akihutubia kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari ni kulinda uhuru wa kupata habari.

(Sauti ya Jan)

Vita na mazingira hatarishi haviwezi kuwa kisingizio cha kuwanyamazisha waandishi wa habari. Badala yake, ni wakati huu hasa ambapo sauti ya wasiokuwa na sauti, na ripoti kutoka vitani zinapaswa kusikika kwa sauti ya juu.” 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la waandishi bila mipaka, Christophe Deloire ameliomba baraza la usalama liunde mfumo wa kuthibitisha utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama kuhusu utunzaji wa waandishi wa habari na kuteua Mwakilishi Maalum kuhusu swala hilo.

Hatimaye, Marianne Pearl mwandishi wa habari na pia mjane wa mwandishi wa mwandishi wa habari Daniel Pearl, amezingatia umuhimu wa kazi ya waandishi wa habari.

(Sauti ya Marianne)

“Mimi na waandishi wengine wengi ambao kamwe hamuwezi kuwasikia, tunafanya tuwezalo kupitia zana ambazo uandishi wa habari zinatupatia kuvunja msingi ambao kwao magaidi wanatumia, yaani chuki. Kwa hiyo tunaripoti kile ambacho chuki inaleta;ujinga, choyo,  rushwa, ulaghai, ukiukwaji wa haki za binadamu, na tabia ya kurahisisha kile ambacho hakiwezi kurahisishwa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter