Maisha ya watoto robo milioni yako hatarini Sudan Kusini: UNICEF

Maisha ya watoto robo milioni yako hatarini Sudan Kusini: UNICEF

Maisha ya watoto takriban 250,000 yako hatarini nchini Sudan Kusini, wakati hali ya usalama wa chakula inazidi kuzorota kwa sababu ya mapigano na mzozo wa kiuchumi.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, ambalo limesema leo kwenye taarifa yake kwamba idadi ya watu wanaokumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula imeongezeka maradufu tangu mwanzo wa mwaka huu nchini Sudan Kusini.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini, Jonathan Veich, amesema licha ya jitihada za UNICEF za kuwasaidia watoto karibu 50,000 walioathirika na utapiamlo mwaka huu pekee, bado maisha ya wanawake na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, bila huduma za chakula na afya, yako hatarini.

Halikadhalika, UNICEF imesema mapigano kwenye maeneo ya Upper Nile yamesababisha angalau watu 100,000 kukimbia makwao, wakitelekeza akiba zao za mazao na mifugo yao, huko baadhi ya mashirika ya kibinadamu yakilazimika kuondoka.

UNICEF imetoa wito wa dola milioni 25 ili kufadhili mradi wake wa kupambana na utapiamlo Sudan Kusini.