Skip to main content

UNDP yahaha kuwajengea nyumba 500,000 za muda raia wa Nepal

UNDP yahaha kuwajengea nyumba 500,000 za muda raia wa Nepal

Mwezi mmoja baada ya tetemeko la kwanza la ardhi lililotokea nchini Nepal tarehe 25 Aprili, mashirika ya kimataifa yanajitahidi kuisaida nchi katika shughuli za ukarabati.

Msaidizi Msimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP Magdy Martinez-Soliman amesema hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York baada ya ziara yake huko Nepal, akisema kipaumbele cha UNDP nchini humo ni kujenga nyumba za muda kabla msimu wa mvua haujaanza.

« Ni kazi inayotisha, kukarabati nyumba nusu milioni, yaani kusaidia familia nusu milioni, kuwalinda na msimu wa mvua unaokaribia, na msimu wa baridi utakaokuja baadaye. Uharibifu ni mkubwa sana, nimeushuhudia mwenyewe, na usaidizi umeendelea kuwa kipindi cha mwezi mmoja lakini bado zaidi inahitajika. Ukarabati utaomba bidii sana.»

Bwana Magdy ameeleza kwamba UNDP inatarajia kujenga upya nyumba za raia na za serikali kwa njia bora zaidi ili uharibifu kama ule usitokee tena.

Ameongeza kwamba serikali inapanga pia kukarabati miundombinu na majengo ya urithi wa dunia ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Nepal.

Aidha amesema UNDP inalenga kurejesha hali ya kiuchumi kupitia miradi ya kuwashirikisha wananchi katika kazi za ujenzi huku wakiwapatia malipo na tayari imeanzisha mradi wa dola milioni 175 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya ukarabati wa maeneo ya shambani.

Hata hivyo aBwana Magdy amesema bado zaidi ya milioni 160 zahitajika.