Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNSOM, Somalia

Baraza la Usalama laongeza muda wa mamlaka ya UNSOM, Somalia

Baraza la Usalama limepitisha leo kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, kwa wiki 10 zaidi hadi tarehe Saba Agosti mwaka huu. Maelezo kamili na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Azimio hilo limeongeza muda wa mamlaka ya UNSOM kwa kipindi cha wiki kumi tu wakati huu ambapo Baraza la Usalama linatarajia kusikiliza ripoti kuhusu uchunguzi uliofanyika kwa pamoja kuhusu kazi ya UNSOM na ujumbe wa Muungano wa AFrika nchini Somalia, AMISOM.

Ripoti hiyo inatakiwa kuwasilishwa tarehe 30 mwezi Mei mbele ya Baraza la Usalama, na muda wa mamlaka ya UNSOM ulikuwa unaisha rasmi tarehe 28 mwezi huu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa UNSOM Nicholas Kay na Mkuu wa  AMISOM, Maman Sidikou, ambao wamelihutubia Baraza la Usalama wiki iliyopita kuhusu matokeo ya awali ya ripoti hii, itakuwa ni lazima kuangalia upya ushirikiano kati ya UNSOM na AMISOM na kubadilisha mgawanyiko wa kazi baina yao.