Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mauaji ya mwanasiasa Zedi Feruzi Burundi

Ban alaani mauaji ya mwanasiasa Zedi Feruzi Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani mauaji ya Bwana Zedi Feruzi, ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Umoja wa Kitaifa na Maendeleo (UPD) Zigamibanga, pamoja na mlinzi wake mnamo siku ya Jumamosi mjini Bujumbura.

Taarifa ya msemaji wake imesema kitendo hicho cha uhalifu, pamoja na shambulizi la gruneti kwenye soko kuu la Bujumbura mnamo Mei 22 lililosababisha vifo vya watu wawili na wengi kujeruhiwa, vinatishia kuchochea kutoaminiana na kuibua machafuko zaidi.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa mamlaka za Burundi kuwafikisha haraka walioutekeleza uhalifu huo mbele ya mkono wa sheria, huku akipeleka rambirambi zake kwa familia za wahanga, na kuwatakia nafuu haraka waliojeruhiwa.

Ban amesema, vitendo hivyo vya ghasia vinakumbusha haja ya viongozi wote wa kisiasa Burundi kuushughulikia mzozo wa kisiasa uliopo sasa kwa njia ya kuwajibika, na kuweka amani na maridhiano ya kitaifa mbele ya matakwa yao binafsi.

Katibu Mkuu ametoa wito pia kuwepo utulivu na kujizuia, na kuzitaka mamlaka za Burundi kuhakikisha haki za binadamu za Warundi wote zinalindwa, ukiwemo uhuru wa kufanya mikutano na kujieleza, na kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya kisiasa na ghasia.