Ban asikitishwa na kutoafikiwa makubaliano kuhusu silaha za nyuklia

23 Mei 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na kongamano la 2015 kuhusu kupinga uenezaji wa silaha za nyuklia kushindwa kufikia makubaliano muhimu.

Katibu Mkuu amesikitishwa hasa na nchi wanachama wa Mkataba wa Kupinga Uenezaji wa Silaha za Nyuklia kushindwa kuondoa tofauti zao kuhusu mustakhbali wa uondoaji wa silaha za nyuklia, au kufikia mtazamo wa pamoja kuhusu jinsi ya kuwa na ukanda wa Mashariki ya Kati usio na silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi ya halaiki.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi zote kuendeleza msukumo zilizoweka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo mikakati mipya inayolenga kuondoa silaha za nyuklia na juhudi endelevu za kuimarisha kutoeneza silaha za nyuklia. Kuhusu Mashariki ya Kati, Katibu Mkuu amesema ataendelea kuwa tayari kuunga mkono juhudi za kuchagiza na kuendeleza mazungumzo jumuishi yanayohitajika kufikia lengo hilo.

Amesema anatumai kuwa kuendelea kuwepo uelewa kuhusu athari za kibinadamu za matumizi yoyote ya silaha za nyuklia kutatoa msukumo kwa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuzuia na kutokomeza silaha za nyuklia.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter