Baraza la Usalama lalaani vitendo vya ISIL Saudia na Syria

23 Mei 2015

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali shambulizi la kigaidi la Mei 22, lililodaiwa kufanywa na kundi linalotaka kuweka dola la uislamu wenye msimamo mkali, ISIL au Da’esh, kwenye msikiti mmoja huko Qatif, Ufalme wa Saudia. Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu wapatao 21.

Katika taarifa iliyotolewa na rais wa Baraza hilo, Raimonda Murmokaitė, wanachama wa Baraza la Usalama wametuma rambirambi zao kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo na kwa serikali ya Saudia.

Wajumbe hao wamekariri tena kuwa ISIL ni lazima ishindwe, na kwamba msimamo mkali, ukatili na chuki linaloeneza kundi hilo, ni lazima vikomeshwe. Wamesema vitendo kama hivyo vya kinyama haviwatishi, bali vinaimarisha ari yao kwamba kunapaswa kuwepo juhudi za pamoja miongoni mwa serikali na taasisi, zikiwemo zile za kikanda, ili kupambana na ISIL na makundi yanayoiunga mkono kama Ansar Al Shari’a.

Aidha, wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamelaani vikali vitendo vya kinyama vinavyotekelezwa na ISIL nchini Syria, vikiwemo kuuteka mji wa Palmyra kwa njia ya kikatili.

Wameelezea wasiwasi wao kuhusu maelfu ya wakazi wa mji huo wa Palmyra, na kuhusu wote waliolazimika kuhama kutokana na vitendo vya ISIL.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter