Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon akaribisha mazungumzo ya siasa Bujumbura

Ban Ki-moon akaribisha mazungumzo ya siasa Bujumbura

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea matumaini yake kuhusu mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea mjini Bujumbura.

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akipongeza washiriki wa mazungumzo hayo kwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, akitaja hatua zilizokubaliwa ili kupunguza mvutano na kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi wenye amani, usawa na uhuru.

Hata hivyo, ameelezea wasiwasi wake kuhusu tatizo la kibinadamu linalowakumba wakimbizi. Ameshukuru nchi jirani kwa ukarimu wao na kuisihi serikali ya Burundi kujenga mazingira yatakayowawezesha kurudi kwao.

Akikariri utayari wa Umoja wa Mataifa wa kuwasaidia raia wa Burundi na ukanda mzima katika utaratibu huu, Katibu Mkuu amependekeza wadau wote waendelee na mazungumzo hayo hadi kufikia mwafaka kuhusu shida zote walizozibaini.

Mazungumzo ya kisiasa ya Burundi yameratibiwa na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Maziwa Makuu Said Djinnit na wawakilishi wa Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, na mashirika mengine ya kikanda, yakishirikisha wawakilishi wa jamii, vyama vya kisiasa, mashirika ya kidini na serikali ya Burundi.