Skip to main content

Ban alaani mashambulizi ya Saudia

Ban alaani mashambulizi ya Saudia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi ya leo Ijumaa  yalioyolenga msikiti wa Shia katika mji wa al-Quidaih katika jimbo la Mashariki la Ufalme wa Saudia.

Mashambulizi hayo yamesababisha vifo na majeraha kwa watu ambao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya sala ya Ijumaa.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemkariri Ban akisisitiza kwamba mashambulizi kama hayo ya maeneo ya ibada hayakubaliki na yana lengo la kuzua mzozo wa kidini huku ikiongeza kwamba anatarajia kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Kadhalika Bwana Ban ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya wahanga huku akionyesha mshikamano wake na serikali na watu wa Ufalme wa Saudia.