Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kuzuia silaha ndogo ndogo

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kuzuia silaha ndogo ndogo

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo wamepitisha azimio kuhusu kupinga usafirishaji haramu na uzagaaji wa silaha ndogo ndogo na nyepesi, likiungwa mkono na wanachama tisa kati ya kumi na watano, wajumbe sita wakiwa hawakuonyesha wanaegemea upande gani.

Katika azimio hilo, wajumbe hao wamehimiza uanzishaji au uimarishaji wa ushirikiano na uratibu wa kikanda kwa minajili ya kuzuia, kupambana na, au kutokomeza usafirishaji na ulimbikizaji, pamoja na matumizi mabaya ya silaha hizo.

Wajumbe hao wamekariri kuwa usafirishaji, ulimbikizaji na matumizi mabaya ya silaha hizo, ni kichochezi cha migogoro na athari zisizoelezeka dhidi ya raia.

Kabla ya kura ya kupitisha azimio hilo, Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Mei, Balozi Raimonda Murmokaitë wa Lithuania, amepaazia sauti waathiriwa wa uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi:

Mnapopiga kura, tafakari kuhusu akina mama wanaoishi katika uoga kuwa waasi, magaidi na magenge ya wanajeshi watavamia nyumba zao na kuiba, kubaka na kuwateka wanao na kuwauza binti zao katika utumwa. Tafakari kuhusu wakimbizi, kuhusu walio wachache kidini wakikimbilia uhai wao, na kuhusu wazee na wenye ulemavu ambao hawezi kukimbia. Tafakari kuhusu watoto wenye umri wa miaka 6 au minane, ambao hata hawawezi kukamata bunduki, wanapotishwa, kupotoshwa na kulazimika kukata viungo, kutesa au kuua ili wapate kuishi.”

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekariri pia wito wao kuwa pande zote katika mizozo ya silaha ni lazima zitimize wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ile ya haki za binadamu na sheria ya kimataifa kuhusu wakimbizi, na kusisitiza kuwa ni lazima pande zinazozozana zichukue hatua kulinda raia.