Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya raia 1000 wa Yemen wameuawa katika wiki 3- UM

Zaidi ya raia 1000 wa Yemen wameuawa katika wiki 3- UM

Raia wa Yemen wapatao 1,030 wameuwawa katika kipindi cha wiki tatu kufikia Mei 20, kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Miongoni mwa waliofariki ni wanawake 130 na watoto 234, huku raia wapatao 2,450 wakiwa wamejeruhiwa.

Mapigano yameanza tena katika taifa hilo, baada ya sitisho la siku tano la kuruhusu kufikisha usaidizi wa kibinadamu, huku mamilioni ya watu wakiwa bado wanahitaji usaidizi wa kibinadamu.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Cécile Pouilly ametoa wito kwa pande zinazopigana ziwalinde raia

"Kutokana na idadi kubwa ya raia waliouawa katika wiki nne zilizopita, tunarejelea kutoa wito kwa pande zote kutimiza wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kuchukua hatua zote ziwezekanazo kuhakikisha kuwa raia wanalindwa.”

Mazungumzo yanayolenga kuutatua mzozo wa kisiasa nchini Yemen yanatarajiwa kuanza tena mjini Geneva mnamo Mei 28, yakiwaleta pamoja wawakilishi wa serikali na waasi.