Ban akutana na Waziri Mkuu Nguyen wa Viet Nam

Ban akutana na Waziri Mkuu Nguyen wa Viet Nam

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekutana na kufanya mashauriano na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisosholisti ya Viet Nam.

Katibu Mkuu alimweleza waziri huyo mkuu kuhusu masuala muhimu ya ajenda ya Umoja wa Mataifa katika mwaka ujao, hususan mashauriano kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na kongamano la Paris kuhusu tabianchi, na wakajadiliana kuhusu kushirikiana ili kupiga hatua katika masuala hayo.

Aidha, Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake kuwa Vietnam itatuma ujumbe wa ngazi ya juu kushiriki kongamano la tatu la kimataifa mjini Addis Ababa kuhusu ufadhili kwa maendeleo.

Kuhusu amani na usalama, Ban ameelezea wasiwasi wale kuhusu hali tete kwenye Bahari ya Kusini mwa China, akitoa wito kwa pande zote kujizuia ili kuepusha utata zaidi.

Ameishukuru Vietnam kwa uungaji wake mkono Umoja wa Mataifa, na kujihusisha kwake zaidi na mifumo ya kuendeleza haki za binadamu.