Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongezeka mapigano Sudan Kusini kunaongeza maafa kwa raia- Zeid

Kuongezeka mapigano Sudan Kusini kunaongeza maafa kwa raia- Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameonya leo Ijumaa kuwa kuongezeka kwa mapigano katika wiki chache zilizopita kati ya vikosi vya serikali na vile vya upinzani nchini Sudan Kusini, kumesababisha ukiukwaji mkubwa na wa kusikitisha wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na ile ya kibinadamu, na kusababisha maafa makubwa kwa raia. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Katika taarifa, Kamishna Zeid amesema, kwa zaidi ya miezi 17, wanawake, wanaume na watoto wamekuwa wakiteseka kutokana na janga lililosababishwa na mwanadamu, wakiishi katika hali zisizofaa kwa binadamu.

Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni mbili wamepokonywa nyumba zao, vitu wanavyotegemea kuishi, usalama wao na kupoteza jamaa zao kwa vifo na usajili wa lazima katika jeshi.

Amesema, katika wiki chache zilizopita, pande kinzani zimeifanya hali iliokuwa tayari mbaya kuwa hata mbaya zaidi, na kuzitaka pande zote kuchukua hatua za kuzuia madhara kwa raia na miundo mbinu, wakiwemo wafanyakazi na majengo ya Umoja wa Mataifa.

.