Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi yaliyojihami yawafurusha raia wa Mali kutoka makwao- OCHA

Makundi yaliyojihami yawafurusha raia wa Mali kutoka makwao- OCHA

Shirika la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, limesema kuwa makundi yenye silaha yamewashambulia na kuwalazimu maelfu ya raia kukimbia makwao na kupora mali zao katika eneo la Timbuktu, nchini Mali.

OCHA imesema kwamba, kwa mujibu wa makadirio ya wadau wa kibinadamu na mamlaka za mikoani, takriban watu 27,000 wamekimbia makwao katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, 20,000 wakifurushwa makwao kutokana na ghasia hizo katika wiki iliopita pekee. Jens Laerke ni msemaji wa OCHA, Geneva.

“Watu waliofurushwa makwo wanaishi katika makazi ya muda au na familia za wenyeji katika maeneo ya watu wengi au karibu na ukingo wa kusini mwa Mto Niger. Wanahitaji kwa dharura maji, chakula, vifaa visivyo chakula na makazi.”

Mashirika ya kibinadamu katika eneo hilo yanajiandaa na vifaa vya misaada, na tayari ugawaji wa msaada wa chakula umeanza. Tathmini pia inafanywa kujua mahitaji kamili, lakini kuzorota usalama katika wilaya ya Gourma Rharous walikotawanyika zaidi ya wakimbizi 15,000 kumetatiza kulifikia eneo hilo.