Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu chaua watu 31 Tanzania, wakiwemo Warundi 29

Kipindupindu chaua watu 31 Tanzania, wakiwemo Warundi 29

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR pamoja na wahisani 17 , leo wametoa wito wa ufadhili wa dola milioni 207 kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi. Taarifa zaidi na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Wito uliotolewa leo unalenga kuwasaidia wakimbizi wa Burundi wanaotafuta hifadhi kwenye nchi jirani, UNHCR ikikadiria kwamba idadi yao inaweza kufikia 200,000.

Wakati huo huo UNHCR limeripoti leo kuwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika eneo la Kagunga karibu na Ziwa Tanganyika, umewaua wakimbizi 29 kutoka Burundi na Watanzania wawili.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

"Vifo vimekuwa katika mji wa bandari ya Kigoma kwenye Ziwa Tanganyika, katika vijiji jirani vya Kagunga na Nyarugusu, na miongoni mwa watu wanaosafirishwa kwa feri kutoka Kagunga kwenda Kigoma. Kufikia leo, visa 3,000 vimeripotiwa, na idadi hiyo inaongezeka kwa visa 300-400 kila siku, hususan kule Kagunga na maeneo jirani. Kwa mwelekeo huu, visa zaidi vinaweza kutarajiwa katika siku chache zijazo hadi hali idhibitiwe.”

Akizingimza na waandishi wa habari mjini Geneva, bwana Edwards amesema kuwa hatua za kuzuia ugonjwa huo kupitia huduma za maji safi na za kujisafi ni muhimu, na kwamba UNHCR inashirikiana na wizara ya afya, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine kutoa huduma hizo pamoja na huduma za afya kwa dharura.