Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi: UNICEF yaanza kudhibiti Kipindupindu na kusaidia wa watoto wakimbizi Kagunga

Burundi: UNICEF yaanza kudhibiti Kipindupindu na kusaidia wa watoto wakimbizi Kagunga

Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limepeleka kwa dharura vifaa vya msaada kwenye mpaka wa Tanzania na Burundi ili kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu miongoni mwa wakimbizi 50,000 wa Burundi, ambao wamekusanyika kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya

(TAARIFA YA GRACE)

UNICEF  imesema vifaa hivyo ni pamoja na maji na vifaa vya kujisafi, afya na lishe, ambavyo vinasafirishwa kutoka Burundi na Tanzania, na sasa inashirikiana na wadau kutoka pande zote za mpaka kuongeza jitihada za kukabiliana na mlipuko huo ambao hadi sasa idadi ya vifo  imeongezeka na kufikia 27.

Wakati huo huo UNICEF inasema asilimia 85 ya wakimbizi wanaoingia Tanzania ni wanawake na watoto na tayari wamebaini 1,000 ambao wamekimbia bila kusindikizwa na mtu wewote.

Sandra Bisin, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa UNICEF Tanzania, akihojiwa na idhaa hii kutoka kambi ya Nyarugusu nchini Tanzania, amesema UNICEF limeshatuma watalaam 30 ili kuwahudumia watoto hao, ambao wako hatarini na kukumbwa na ukatili wa aina mbali mbali.

(Sauti ya Sandra)

“ Ni muhimu kuelewa kwamba kabla ya kukimbia Burundi, watoto wakimbizi wengi walikuwa wameshafanywa au kushuhudia ukatili. Wengi wao bado wameshtuka, kwa hiyo kipaumbele chetu ni kuwapatia sehemu salama na kuwawezesha kurejesha hali ya kawaida."

Miongoni mwa watoto hao ni Celeste, mvulana mwenye umri wa miaka 13.

(Clip ya Celeste)

Amesema tayari wameandaa pahala salama huko Kagunga ili watoto waweze kucheza na wenzao na kutunzwa dhidi ya ukatili, na kwamba sehemu nyingine itajengwa kwenye kambi ya Nyarugusu.

Machafuko nchini Burundi yamewalazimu zaidi ya watu 110,000 kukimbilia nchi jirani za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.