Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP yaridhika na mafanikio katika utunzaji wa mazingira mwaka 2014

UNEP yaridhika na mafanikio katika utunzaji wa mazingira mwaka 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP limezindua leo ripoti yake ya mwaka ikimulika mafanikio yaliyopatikana duniani kote mwaka 2014, ikiwemo kuanza kurejea kwa tabaka la ozoni lililokuwa limeanza kumomonyolewa na hewa chafuzi.

Katika taarifa yake, UNEP imekaribisha mafanikio hayo ikisema ni matokeo ya mkataba wa Montreal wa mwaka 1987 uliokataza matumizi ya gesi zinazoharibu tabaka la ozoni, na kuongeza kwamba mafanikio hayo yameweza kuzuia mamia ya milioni ya visa vya saratani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, eneo lingine la kuridhika ni ongezeko la uwekezaji katika nishati endelevu, hasa kwenye nchi zinazoendelea, ambapo ongezeko hilo limefikia asilimia 36 mwaka 2014.

Ripoti imetaja mfano wa nishati itokanayo na joto ardhi ambayo inazalishwa nchini Kenya kwenye maeneo ya Olkaria, ambapo matarajio ya serikali ya nchi hiyo ni kuzalisha theluthi moja ya nishati kutoka joto ardhi ifikapo mwaka 2030.