Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mapigano mapya na uhalifu Sudan Kusini

Ban alaani mapigano mapya na uhalifu Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali kuongezeka kwa mapigano katika siku kumi zilizopita baina ya jeshi la serikali ya Sudan Kusini (SPLA) na lile la SPLA upinzani na vikosi vinaovyoyaunga mkono katika majimbo ya Unity na Upper Nile.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu Mkuu akielezea kusikitishwa na ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na jeshi la SPLA na vikosi vinavyoliunga, ukiwemo uchomaji wa vjiji, pamoja na kuwaua na kuwabaka raia wakati wa operesheni za kijeshi katika jimbo la Unity.

Amelaani pia mauaji ya raia wanne wakimbizi wa ndani waliojikuta katikati ya ufyatulianaji risasi katika ua la kituo cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS huko Melut. Ametaka uchunguzi wa kitaifa ufanywe mara moja ili wale waliotekeleza uhalifu huo wawajibishwe na viongozi wao.

Ban amesisitiza kuwa mapigano hayo hayakubaliki, na kwamba ni sehemu ya msururu wa ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha uhasama yaliyosainiwa mnamo Januari 23 2014, na pia yanaonyesha kutoheshimu juhudi zinazofanywa na IGAD za kutafuta suluhuisho la kisiasa kwa mzozo wa Sudan Kusini.