Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waonya Israel dhidi ya uhamisho wa Wapalestina.

Umoja wa Mataifa waonya Israel dhidi ya uhamisho wa Wapalestina.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu kwa maeneo yaliyokaliwa ya Palestina, James W. Rawley na Mkurugenzi wa operesheni za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kwa Ukingo wa magharibi wa mto Jordan, Felipe Sanchez, wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu mpango wa Israel wa kuhamishia wapalestina mabedui kwenda katikati ya ukingo huo wa magharibi.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo, viongozi hao wawili wamesema jamii hiyo ya wapalestina mabedui ambayo idadi yao ni takriban watu 7,000, wamearifiwa tarehe 28 Aprili, kuwa wanapaswa kujiandaa kuhamia kwenye eneo lingine lililotayarishwa na Israel.

Bwana Sanchez ameeleza kwamba wanahofia kuwa uhamisho huo utawezesha Israel kujenga makazi mengine yasiyokuwa halali kwa walowezi.

Naye Bwana Rawley amesema uhamisho huo utaathiri mila na maisha ya mabedui hao, wakati waisraeli watazidi kujenga kwenye maeneo hayo yaliyokaliwa na kuhatarisha zaidi uwezekano wa kupata suluhu ya mataifa mawili.

Bwana Rawley na Bwana Sanchez wameisihi Israel kusitisha mpango huo wa uhamisho.