Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa wa jinsia kwenye sekta ya uvuvi kuimarisha usalama wa chakula:FAO

Usawa wa jinsia kwenye sekta ya uvuvi kuimarisha usalama wa chakula:FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linashirikiana na mashirika, vyama vya ushirika wa uvuvi na vyuo vikuu kuanzisha mtandao wa wanawake katika sekta ya uvuvi.

Lengo la mtandao  huo ni kuibua wanawake kwenye uongozi wa sekta hiyo na kuwavutia wengine ili kuimarisha uwepo zaidi wa wanawake wakati huu ambapo ripoti mpya ya FAO imeonyesha kubinywa kwa usawa wa ujinsia na wanaume kushamiri zaidi.

Kwa mujibi wa ripoti hiyo, wakati wanawake wanakadiriwa kuwa nusu ya wahusika kwenye sekta ya uvuvi, bado majukumu yao yanasalia kuwa yasiyo muhimu na hivyo kukwamisha maendeleo yao endelevu na hata ya familia zao.

Mathalani imeelezwa kuwa wanaume wanahusika zaidi katika uvuvi na umiliki wa viwanda ilhali wanawake wanajikuta katika usafishaji wa mashua, usafishaji wa samaki na hata uchuuzi wa kiwango cha chini ambao ujira wake ni mdogo na wakati mwingine  hakuna kabisa.

Ripoti hiyo inasema licha ya kwamba sekta ya uvuvi ni tegemeo kwa watu zaidi ya milioni 120 duniani kote, pia samaki ni chanzo cha virutubisho vya afya hivyo uwepo wa usawa wa jinsia ni muhimu pia kwa kipato na usalama wa chakula.