Baraza la Usalama lakutana kuhusu Yemen, Ban atangaza tarehe ya mazungumzo

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Yemen, Ban atangaza tarehe ya mazungumzo

Baraza la Usalama limekutana leo kwenye kikao cha faragha ili kujadili hali ya Yemen, huku mapigano yakiwa yameanza tena baada ya kuisha kwa kipindi cha siku tano cha sitisho la mapigano. Taarifa zaidi na Assumpa Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kikao hicho kimehutubiwa kwa njia ya video na Mjumbe maalum mpya wa Umoja wa Mataifa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, ambaye amehudhuria mkutano wa Baraza la Ushirikiano kwa Ghuba, GCC, kuhusu Yemen, uliofanyika mjini Riyadh wiki hii.

Aidha wanachama wa Baraza la Usalama wamesikiliza kutoka kwa mkurungezi wa operesheni za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, John Ging, ambaye amewaelezea kuhusu hali ya binadamu wakati tayari watu 1,820 wameuawa na wengine 545,000 wamelazimika kuhama makwao nchini Yemen.

Mkutano huo umefanyika wakati ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza kuwa mazungumzo ya kisiasa yataanza tena Mei, 28, mjini Geneva, akisema ni lazima utaratibu huo wa kisiasa uwe jumuishi, wenye amani na kuwa utaongozwa na Wayemen.