Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha usaidizi kwa wahamiaji huko rasi ya Bengal

UNHCR yakaribisha usaidizi kwa wahamiaji huko rasi ya Bengal

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR) limekaribisha azma iliyotangazwa leo na mawaziri wa mambo ya nje wa Malaysia, Indonesia na Thailand ya kupatia suluhu sintofahamu dhidi ya maelfu ya wahamiaji na wakimbizi walioko kwenye boti kadhaa huko rasi ya Bengali, kwenye pwani ya kusini-mashariki mwa Asia.

Taarifa ya UNHCR imesema tangazo hilo ni hatua muhimu katika kupatia suluhu suala hilo kwa mustakhbali wa maisha ya wananchi hao.

Kwa mantiki hiyo limesema jambo muhimu sasa ni watu hao kufikishwa pwani kutoka baharini bila kuchelewa na usaidizi wa haraka ufanyike kwa wale wenye mahitaji ya dharura.

UNHCR imesema inaridhia wito wa mawaziri hao kuwa hatua zaidi zinahitajika ikiwemo kushughulikia chanzo cha hali hiyo na kuzingatia mahitaji ya wale wanaotaka ulinzi wa kimataifa.

Kwa mujibu wa UNHCR, kwa sasa duniani kuna mwelekeo mkubwa wa wasaka hifadhi kusafiri kwa bahari hivyo ni vyema nchi na kanda mbali mbali kushirikiana ili kushughulikia suala hilo kwa ufasaha na kwa mafanikio.