DPRK yasitisha ziara ya Ban huko Kaesong, Katibu Mkuu asikitishwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza masikitiko yake kufuatia tangazo la serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK la kubadili mpango wa ziara yake kwenye eneo huru la viwanda huko Kaesong. Taarifa ya Amina Hassan inafafanua zaidi.
(Taarifa ya Amina)
Ban amesema hayo wakati akifungua kongamano la digitali mjini Seoul, Korea Kusini ambapo amesema wamepatiwa taarifa hizo kupitia vyanzo vya kidiplomasia vya DPRK na kwamba hakuna maelezo yoyote kuhusu uamuzi huo uliotolewa leo asubuhi.
(Sauti ya Ban)
“Uamuzi wa Pyongyang unasitikisha sana. Hata hivyo mimi kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sitaacha jitihadayoyote ya kuisihi DPRK kushirikiana na jamii ya kimataifa kwa ajili ya amani na utulivu kwenye rasi ya Korea na kwingineko.”
Bwana Ban alikuwa afanye ziara hiyo kesho Alhamisi kwenye eneo huru la viwanda la Kaesong lililoko DPRK ambalo ni mradi unaodhihirisha manufaa ya ushirikiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini.
Ingalikuwa ni ziara ya kwanza kufanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 20.
Akiwa mjini Seoul, Katibu mkuu pia ametunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa katika chuo cha masuala ya wanawake.