Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani Mashariki ya Kati inawezekana tu kwenye meza ya mazungumzo- Mladenov

Amani Mashariki ya Kati inawezekana tu kwenye meza ya mazungumzo- Mladenov

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, amesema kuwa ukanda wa Mashariki ya Kati unakumbana na wimbi la ugaidi na misimamo mikali, ambalo linaweka changamoto kubwa mno kwa ukanda huo na kwa amani na usalama wa kimataifa.

Bwana Mladenov amesema hayo Jumanne jioni, wakati akilihutubia Baraza la Usalama ambalo limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati.

Mladenov amesema kuwa kushindwa kuitikia matakwa halali ya ndoto za watu wa Palestina na matakwa ya kiusalama ya Israeli kwa kipindi cha miaka 60, kumechochea hali ambayo inazidi kuwa hatarishi kila uchao.

Amesema kuwa vizazi vya watu wa Palestina na Israel vimetambua kuwa, kufikia amani endelevu na haki hakuwezi kutimizwa kupitia migogoro, bali kupitia mazungumzo. Amesema maelfu ya watu wamefariki dunia, na hivyo kuthibitisha kauli kuwa, amani haiwezekani kupitia machafuko, ila kwenye meza ya mazungumzo.