Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Mashariki ni ukanda unaokuwa zaidi kiuchumi barani Afrika

Afrika Mashariki ni ukanda unaokuwa zaidi kiuchumi barani Afrika

Ripoti mpya iliyotolewa leo na idara ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa, DESA inatarajia kuwa ushirikiano wa kikanda, uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, miundombinu, mawasiliano na teknolojia utasaidia ukuaji wa uchumi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufika asilimia 6.8 kwa mwaka 2015, ukanda wa Afrika ya Mashariki ukiwa ukanda unaokuwa kwa kasi zaidi barani Afrika.

Ripoti hiyo ya katikati ya mwaka kuhusu hali ya uchumi duniani inaonyesha kuwa ukuaji wa kiuchumi duniani kote bado unaendelea kwa kasi ndogo zaidi kuliko kasi ya kabla ya mzozo wa kiuchumi wa 2008.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini New York wakati wa uzinduzi wa ripoti, Pingfan Hong, mtalaam wa uchumi wa DESA ameeleza kwamba uchumi unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.8 mwaka 2015, na unatarajiwa kuongezeka pole pole mwaka 2016 hadi 3.1% mwaka 2017.

Bwana Hong amemulika ongezeko la tofauti baina ya nchi, baadhi ya nchi zikiathirika na kuporomoka kwa bei ya mafuta, na bidhaa zingine.

« Hali ya kiuchumi kwa sasa, kwa kiasi kikubwa inatambuliwa na ukuaji mdogo wa kiuchumi, kiwango kidogo cha biashara, uwezekaji mdogo, riba ndogo na mfumuko mdogo wa bei, pamoja na kwenye nchi nyingi kiwango cha juu cha masoko ya hisa na kiwango cha juu cha madeni. Takwimu hizo zote pamoja ni viashiria vibaya kwa ukuaji wa uchumi katika miaka ijayo iwapo viongozi wa dunia hawatasitisha mwelekeo huo. »