Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa ufadhili watishia usaidizi kwa wanaokimbia Ramadi, Iraq

Uhaba wa ufadhili watishia usaidizi kwa wanaokimbia Ramadi, Iraq

Ofisi ya kuratibu maswala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa kufikia Mei 18, watu wapataoo 25,000 walikuwa wamekimbia mji wa Ramadi kufuatia mashambulizi ya ISIL na mapigano mjini humo.

OCHA imesema, wengi wa waliolazimika kukimbia makwao wanaelekea mji wa Baghdad, wengi wao wakijaribu kuingia kupitia vituo vya upekuzi wa kiusalama.

Kwa mujibu wa OCHA, Umoja wa Mataifa unajitahidi kuwafikishia haraka misaada watu hao wanaokimbia wimbi jipya la mapigano, lakini fedha zinadidimia na akiba ya misaada pia inakaribia kuisha.

Ofisi hiyo imeonya kuwa, iwapo fedha za usaidizi hazitapatikana, programu 56 za afya nchini Iraq zitalazimika kufungwa ifakapo mwezi Juni, nyingi zikiwa kwenye maeneo waliko wakimbizi; na ifikapo Julai, utoaji msaada wa chakula utakatizwa iwapo fedha hazitapokelewa kwa dharura.