Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon kuzuru Korea Kaskazini

Ban Ki-moon kuzuru Korea Kaskazini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiendelea na ziara yake huko Jamhuri ya Korea, ametangaza rasmi kuwa atatembelea Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, , siku ya alhamis, akiwa ni Katibu Mkuu wa kwanza kuzuru nchi hiyo katika kipindi cha miaka 20.

Ameeleza kwamba atatembelea eneo huru la viwanda, akisema eneo hilo ni mradi unaonyesha faida ya kushirikiana baina ya Korea hizo mbili.

Bwana Ban amesema hayo akizungumza leo na waandishi wa habari baada ya kufungua rasmi kongamano la Kimataifa la Elimu, mjini Incheon, Jamhuri ya Korea.

Amesisitiza umuhimu wa kurejesha mazungumzo baina ya Jamhuri ya Korea na DPRK, akisema Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia katika mazungumzo na kukuza utawala wa sheria na haki za binadamu.

(Sauti ya Ban Ki-moon)

« Amani na Usalama kwenye ya rasi ya Korea vimekuwa daima kipaumbele changu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Naamini nguvu ya mazungumzo. Ili kukabiliana na changamoto zilizopo kati ya pande mbili za Korea, mazungumzo ndio njia ya pekee ya kusonga mbele”

Katika hatua nyingine, akizungumza na viongozi wa sekta ya uchumi kutoka mtandao wa Global Compact, Bwana Ban amewapongeza kwa juhudi za Jamhuri ya Korea katika ukuaji wa kiuchumi na uvumbuzi kwenye sekta ya teknolojia, akizingatia umuhimu wa kuwajibika katika maswala ya mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijamii.